1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kukopa Benki ya Dunia, IMF kupunguza bei za mafuta

Iddi Ssessanga
10 Mei 2022

Tanzania iko katika hatua za mwisho kupata mikopo kutoka Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF kuisaidia kupunguza gharama zinazoongezeka za maisha, amesema waziri wa nishati Januari Yusuf Makamba.

https://p.dw.com/p/4B6Sx
Tansania Budget
Picha: DW/Kizito Makoye Shigela

Waziri Makamba amesema wakati akitangaza ruzuku ya mafuta ya dola milioni 43 itakayoanza Juni, kwamba serikali imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini.

Waziri Makamba ambaye alikuwa akitoa tamko la serikali bungeni kuhusu kupanda kwa gharama za maisha, kwamba ruzuku hiyo inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka2021/22.

Soma pia: Tanzania, Uganda zakubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji

"Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali. Ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini.

Tansania January Makamba
Waziri wa nishati wa Tanzania, Januari Yusuf Makamba.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

"Ruzuku hii ya Sh100 bilioni itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa” amesema Makamba.

Soma zaidi: Tanzania:Kuchukua hatua kukabiliana na hali ngumu ya maisha

Makamba amesema nafuu nyingine ya bei ya mafuta itatokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa, IMF. Amesema mchakato wa kuchukua mkopo huo uko mbioni kukamilika na ahueni kwenye kupanda kwa bei za bidhaa itapatikana katika mwaka ujao wa fedha.

Awali Rais Samia Suluhu Hassan alihutubia taifa ambapo alisema serikali itatekeleza maagizo ya bunge ya kutafuta njia za kuwapunguzia makali ya maisha raia kutokana na kupanda kwa bei za nishati ya mafuta, kunakoelezwa kusababishwa na vita vinayoendelea nchini Ukraine.